Sunday, November 10, 2013

Vita kali ya usajili Simba, Yanga

NA ABDUCADO EMMANUEL

KITENDO cha Yanga SC kumsajili kipa wa zamani wa Simba SC, Juma Kaseja, kimeonesha kuamsha vita kali ya usajili miongoni mwa timu hizo, lengo likiwa ni kubomoana.

Kwa mujibu wa kalenda ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), inaonesha kuwa dirisha dogo la usajili litafunguliwa rasmi Ijumaa ijayo na kufungwa Desemba 15 mwaka huu.

Ijumaa iliyopita saa 2 usiku, Yanga ilifanikiwa kuinasa saini ya Kaseja, kwa dau la Sh milioni 40, kwa mkataba wa miaka miwili, ambapo waliwapiku wapinzani wao wa jadi Simba, ambayo nayo ilikuwa vitani kumwania.

Simba ilipanga kumrudisha kundini, Kaseja licha ya kumnyima mkataba mpya msimu huu, kutokana na kipa  Mganda, Abel Dhaira kuboronga kwa kufungwa mabao ya kizembe kwenye mechi mbalimbali alizoichezea timu hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa za ndani kutoka Simba, zinasema kuwa mara baada ya Kaseja kusajiliwa Yanga, klabu hiyo imekuwa na vikao vizito juzi na jana ambapo wametoka na azimio la kuibomoa klabu ya Yanga.

“Baada ya kumkosa Kaseja, hivi sasa tutapambana kumsajili kipa aliyekalia kuti kavu ndani ya Yanga, Ally Mustafa ‘Barthez’, ili kuimarisha nafasi ya kipa ambayo imepwaya,” kilisema chanzo hicho.

Simba inaweza kufanikiwa kwenye jaribio lake hilo, kutokana na Barthez kuwa mbioni kutimka Yanga, kufuatia kuandamwa na mashabiki mara kwa mara, baada ya matokeo ya sare ya mabao 3-3 dhidi ya Simba, wakidai alihujumu mechi hiyo na kuachia mabao kizembe.

Pia suala la kuwekwa benchi nalo linachangia kwenye mbio hizo za Barthez kutaka kuikacha Yanga, huku akiona giza zaidi mara baada ya kutua kwa Kaseja, kwani aliwahi pia kumkimbia akiwa Simba kutokana na kuwekwa kwake benchi.

“Kama hiyo (kumchukua Barthez) haitoshi, tumepanga kuibomoa Yanga kwa kuchukua mshambuliaji wao mmoja ambaye ni noma kwa kupachika mabao hivi sasa, ila hatuko tayari kutangaza kwa sasa,” kilizidi kueleza chanzo hicho

Katika kuhakikisha wamedhamiria kuitikisa Yanga, tayari wameingia kwenye vita ya kumwania kiungo wa timu ya Ruvu Shooting, Hassan Dilunga, ambaye pia anawaniwa na Wanajangwani.

Simba imepanga kumsajili ili kuziba pengo la Haruna Moshi ‘Boban’ aliyehamia Coastal Union msimu huu.

Mbali na majina hayo pia lipo jina la kiungo mshambuliaji wa Yanga, Simon Msuva, ambaye naye anateswa na mashabiki wa Yanga, ambao humzomea kila akiwa dimbani, hii ni kutokana na kutomwamini kinda huyo aliyetokea Ruvu Shooting, huku pia suala la kuwa na mapenzi na Simba likionesha kumtesa zaidi.

Hali kama hiyo inamkumba kiungo mshambuliaji wa Simba, Harun Chanongo, ambaye aliondoshwa kikosini mara baada ya kuboronga kwenye mechi dhidi ya Yanga, akihusishwa na mapenzi ya dhati aliyokuwa nayo kwa Yanga.

Ambapo inasemekana ni mmoja wa wachezaji aliyehusika kuihujumu Simba kwenye mechi hiyo, kufuatia kocha wa timu hiyo, Abdallah ‘King’ Kibadeni kukiri baadhi ya nyota wake kuhusika. Inaelezwa kuwa nyota huyo amepanga kutimkia Yanga ili kuondokana na hali hiyo inayoendelea kumtesa, baada ya kuwekwa kando kwenye kikosi cha Simba.

Hii si mara ya kwanza kwa Simba na Yanga, kuvurugiana mipango ya usajili pamoja na kubomoana vikosi vyao, kwani msimu uliopita Yanga iliibomoa Simba, kwa kumsajili beki wake kisiki Kelvin Yondani, huku Simba ikimsajili beki wa Yanga, Amir Maftah misimu miwili iliyopita.

0 comments:

Post a Comment