Sunday, August 4, 2013

Wabunge wagombea Sh milioni 1

Wakongwe wakijiandaa kwa kabumbu

NA JOHN MADUHU, MWANZA
WABUNGE wawili wa Kanda ya Ziwa, wameingia katika mzozo wa kugombea shilingi milioni moja.
Wabunge hao ni Lameck Airo wa Jimbo la Rorya mkoani Mara (CCM) na Ezekiel Wenje wa Jimbo la Nyamagana mkoani Mwanza.

Akizungumza na MTANZANIA Jumatano jana kuhusu chanzo cha mzozo huo, Airo alisema anamtaka Wenje amrejeshee Sh milioni moja, alizompatia kwa ajili ya harambee ya kuchangia Shule ya Msingi ya Buchili wilayani Rorya, kwa sababu amezitumia badala ya kwenda kutoa mchango.

Airo alisema Wenje alikwenda kumuomba Sh milioni 5 mwishoni mwa wiki iliyopita alizodai kuwa ni mchango kwa ajili ya ujenzi wa Shule ya Buchili pamoja na ununuzi wa madawati na kumtaka ahudhurie harambee hiyo, lakini ratiba yake haikumruhusu hivyo alimpatia Sh milioni 1 ya mchango.

Alisema alishangazwa na taarifa alizopata kutoka kwenye harambee hiyo, kuwa Wenje hakutoa mchango aliompatia na badala yake alitoa maneno ya kashfa dhidi yake pamoja na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Rorya, Charles Ochere, ambaye naye alimchangia kiasi cha Sh 500,000.

Alilalamika kuwa kitendo cha Wenje kutafuna fedha zake ni cha kihuni na kumtaka azirejeshe huku akimtahadharisha kuacha kumchafua katika majukwaa na badala yake washindane katika kuwaletea maendeleo wananchi.

“Nimempatia fedha kwa ajili ya harambee kiasi cha Sh milioni moja na Mwenyekiti naye alitoa Sh 500,000, kwanini hakutangaza mchango wetu katika harambee hiyo na badala yake yeye binafsi alitoa milioni moja pekee bila kutaja tulizompatia, inatia aibu kwa Mbunge kuchukua fedha kwa wabunge wenzako bila kuzifikisha kunakohitajika, kama alikuwa anataka kuongezea mtaji kwa ajili ya duka lake la madawa ni afadhali angetueleza,” alisema Airo.

Aidha Airo alieleza kusikitishwa na kauli iliyotolewa na Mbunge huyo katika harambee hiyo, kuwa amekuwa akimsaidia mambo kadhaa wakiwa bungeni mjini Dodoma na kueleza kuwa huo ni uongo.

Alipotafutwa Wenje kupitia simu yake ya kiganjani kuzungumzia tuhuma hizo, iliita bila kupokelewa.

0 comments:

Post a Comment