Sunday, November 10, 2013

Familia yampeleka Kaseja Yanga

NA EZEKIEL TENDWA

LICHA ya Juma Kaseja kuwa radhi kujiunga na timu yake ya zamani, Simba baada ya mzunguko wa kwanza kumalizika, kikwazo kikubwa kilikuwa kwa familia yake iliyomtaka kujiunga na Yanga.

Familia ya Kaseja ilifikia uamuzi huo baada ya Simba kumtema kipa huyo na nahodha ya timu ya Taifa, ‘Taifa Stars’ kabla ya msimu huu kuanza licha ya kuichezea kwa mafanikio makubwa tangu ajiunge nayo.

Tayari Kaseja amesaini mkataba wa miaka miwili Yanga baada ya benchi la ufundi kumpendekeza asajiliwe wakiamini ataiokoa timu hiyo katika michuano ya kimataifa inayowakabili, kutokana na kipa huyo kuwa na uzoefu mkubwa.

Kabla ya kusajiliwa na Yanga, viongozi wa Simba walitaka kumrudisha katika dirisha dogo lakini familia yake ilimsihi asirudi tena kwenye timu hiyo na badala yake aende kwa watani wao wa jadi Yanga hatua ambayo Kaseja aliitekeleza.

Simba ilimuacha Kaseja kwa madai ya kushuka kiwango, wakiwa na jeuri ya kumtumia, Abel Dhaira na Andrew Ntala ambao hata hivyo wameonekana kutokuwa makini kama Kaseja.

Hii ni mara ya pili Kaseja kusajiliwa na mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Bara, ambapo kabla ya hapo alishaichezea timu hiyo msimu 2008/09 na baadaye kurejea tena Simba.

Baada ya kusajiliwa na Yanga, Kaseja anaungana na magolikipa wawili wa timu hiyo, Ali Mustafa ‘Barthez’ pamoja na Deogratias Munish ‘Dida’ ambao wote wamewahi kuichezea Simba kabla ya kujiunga na Yanga.

0 comments:

Post a Comment