Saturday, August 3, 2013

Hasheem Thabiti: Balozi wa kikapu nchini aliyekumbukwa na Obama

Na Markus Mpangala, Dar es Salaam

Hasheem alipokuja nchini mwake hivi karibuni
DIKEMBE Mutombo ni jina maarufu sana Afrika na duniani kote, kutokana na uwezo wake wa kucheza kikapu. Lakini jina lake kamili ni Dikembe Mutombo Mpolondo Mukamba Jean-Jacques Wamutombo.

Nyota huyo ana sifa kubwa kutokana na alivyoweza kusaidia ukuzaji wa mchezo huo, katika bara la Afrika hususani nchini mwake Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Mutombo kama anavyofahamika, alikuwa akicheza Ligi ya kulipwa ya Kikapu nchini Marekani, kwenye timu ya Houston Rockets. Kwa bara la Afrika mchezo wa Kikapu unapendwa zaidi kwenye nchi za Angola, Morocco na Nigeria pamoja na Tanzania, ambazo kwa nyakati tofauti zimekuwa na ufanisi kwa wachezaji wake.

Tunamkumbuka Mutombo kama tunavyofanya kwa Hasheem Thabiti, ambaye amekuwa akicheza Ligi ya Kulipwa ya Kikapu katika timu ya Oklahoma City Thunder ya Marekani.

Watanzania tunatakiwa kujivunia nyota huyo, ambaye amekuwa na mchango mkubwa wa maendeleo ya mchezo wa kikapu hapa nchini na kuonyesha kila dalili za kufuata nyayo za Dikembe Mutombo, ambaye aliisaidia sana nchi yake.

Bahati nzuri pia, ziara ya Rais Barack Obama, imefungua masikio ya wengi kuwa anatambua kuwa tunaye mchezaji mahiri nchini mwake. Katika mazungumzo yake na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Rais Obama alisema kuwa anatambua kuwa nchi yetu inaye mchezaji kikapu, na hivyo kufanya mazungumzo ya kipekee na mwenyeji wake Rais Kikwete.

Kwa namna nyingine, kauli ya Rais Obama inatukumbusha kuwa kuna uwezekano mkubwa sana, sekta ya michezo hususani mchezo wa kikapu ikanufaika zaidi na matembezi yake ya kikazi.

Tunakumbuka kuwa klabu ya Seattle Sounder ya Marekani, ilimchukua winga Mrisho Ngassa wakati akichezea Azam, ili kufanya majaribio klabuni hapo.

Tuliona Ngassa akicheza mechi ya kirafiki dhidi ya Manchester United. Tunafahamu kuwa Seattle Sounders iliingia ubia na klabu ya African Lyon ya hapa nchini, ili kuendeleza michezo, huku Azam nayo ikiwa mshirika mzuri.

Ziara ya Obama ambayo inamkumbuka nyota wetu Hasheem Thabiti, bila shaka inafungua milango zaidi kwa wachezaji wa mpira wa kikapu na sekta ya michezo kwa ujumla.

Rais Kikwete amekuwa na juhudi za kuendeleza michezo, tangu nia ya kuialika klabu ya Real Madrid, pamoja na mikakati ya sasa ya kuanzishwa akademi ambayo itaishirikisha klabu ya Sunderland ya England.

Ziara ya Obama na kutajwa kwa Hasheem Thabiti, kuna maana moja kuwa rais huyo anatambua kuwa Tanzania imejaliwa vipaji, ndiyo maana mchezaji huyo amekuwa miongoni mwa nyota waliosajiliwa na timu ya kulipwa za ligi ya NBA nchini Marekani.

Kuna kitu kimoja muhimu cha kukiangalia hapa, Obama ametembelea mitambo ya kufua umeme ya kampuni ya Symbion, ambayo ni mshirika wa klabu ya Sunderland.

Kwa maana hiyo ushirika huo kwa wanamichezo, utaleta manufaa makubwa, kwani kwenye mazungumzo yake Rais Obama ameeleza kutambua umuhimu wa Thabiti.

Bila shaka, juhudi zilizofanywa na Thabiti katika kuendeleza mchezo huu, na kwa kuwa alishawahi kukutana na Rais Kikwete mara kadhaa, sasa nyongeza itakuwepo na sekta ya michezo itapata mwamko mpya.

Ni rahisi kutumia ziara hii kuanzisha ushirikiano wa Sunderland, Symbion na Oklahoma City Thunder, ili kuupa kipaumbele mchezo wa kikapu kote nchini, ikiwezekana zaidi ya kipindi cha utawala wa Jackson Kalikumtima.

Tunafahamu tangu kuondoka kwa Jackson Kalikumtima, mchezo wa kikapu haukuwahi kupiga hatua kubwa, lakini kwa ziara ya Rais Obama, ni muhimu kwa wadau wa mchezo huo kusaka njia mbadala ya kuboresha zaidi.

Kwa hakika Thabiti ni balozi wetu wa mchezo wa kikapu, ambaye amekumbukwa na Rais Obama. Sote tujenge taifa letu na ni wakati wa wadau wa mchezo wa kikapu, kuongeza maarifa zaidi ya maendeleo.

0 comments:

Post a Comment