Sunday, November 10, 2013

Kung Fu Mbagala kufanya mashindano mara kwa mara

NA ZAINAB IDDY

UONGOZI wa klabu ya Kung Fu ya Mbangala jijini Dar es Salaam, umepanga programu ya kufanya mashindano ya mara kwa mara, kwa lengo la kuendeleza mchezo huo nchini.

Abdallah Nyoni ni Katibu Mkuu wa klabu hiyo, aliliambia BINGWA kwamba mashindano hayo yatasaidia kupata vipaji ambavyo vitawasaidia katika mashindano mbalimbali.

“Hiyo ni moja ya maandalizi ya kuwaandaa wachezaji kwa ajili ya mashindano mbalimbali mwakani, hivyo tunajipanga mapema,” alisema.

Alisema mwakani kutakuwa na mashindano mbalimbali ndani na nje ya nchi, ndiyo maana wameamua kutengeneza timu yao kupitia mashindano hayo.

Nyoni alisema mbali na programu hiyo, kutakuwa na mazoezi ya kila wiki ambayo yatawawezesha wachezaji kujiweka sawa na kuwa tayari muda wowote kushiriki michuano itakayoandaliwa na klabu nyingine.

“Tutahakikisha tunakuwa mfano wa kufanya vema katika mchezo huo nchini, ndiyo maana tunafanya mambo yote hayo,” alisema.

0 comments:

Post a Comment