Sunday, November 10, 2013

Tambwe mguu ndani, nje Simba

NA ZAINAB IDDY


MSHAMBULIAJI wa Simba, Amisi Tambwe amesema hana muda mrefu kuitumikia Simba, kwani ameanza mazungumzo na timu moja ya Saudi Arabia.

Tambwe aliyasema hayo juzi kwenye mazungumzo maalumu saa chache kabla ya kuelekea Bujumbura, Burundi, baada ya kumalizika kwa mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu Bara.

Alisema kuna uwezekano mkubwa akavunja mkataba na Simba na huenda asionekane katika kikosi hicho katika  mzunguko wa pili, endapo mazungumzo kati ya meneja wake, Alphonce George Twagilamungu yatakwenda  vizuri na timu hiyo ya Saudi Arabia.

“Kuna taarifa nimezipata kutoka kwa meneja wangu, kuna timu imevutiwa na kiwango changu kutoka Saudi Arabia, ila bado tupo kwenye mazungumzo,” alisema.

Tambwe alisema anataka kutumia muda huu wa mapunziko akiwa Burundi, kukutana na meneja wake ili kujua hatima ya uwepo wake Simba.

“Kazi yangu ni mpira, hivyo nipo tayari kucheza katika timu yoyote itakayonihitaji ili mradi timu husika ifuate taratibu za mahali nilipo na itimize yale ninayoyahitaji,” alisema.

Mrundi huyo alisajiliwa na Simba msimu huu kwa mkataba wa miaka miwili akitokea klabu ya Vital’O ya Burundi, ambapo ameonesha uwezo mkubwa katika mzunguko wa kwanza uliomalizika hivi karibuni.

Tambwe ni kinara wa upachikaji wa mabao Ligi Kuu Bara msimu huu, ambapo hadi mzunguko wa kwanza unamalizika, straika huyo ametikisa nyavu mara 10.

0 comments:

Post a Comment