Sunday, November 10, 2013

Kocha Mgambo JKT alia na wachezaji

NA SALMA JUMA

KOCHA mkuu wa timu ya Mgambo JKT, Mohamed Kampira ameweka wazi sababu iliyopelekea timu yake kufanya vibaya katika mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu Bara msimu huu, kuwa ni kuondoka kwa baadhi ya wachezaji wake aliokuwa nao katika ligi iliyopita.

Mgambo wanashikilia mkia kwenye msimamo wa ligi hiyo wakiwa na jumla ya pointi 6, baada ya kushinda mchezo mmoja, kutoka sare mechi tatu na kupoteza mechi 9.

Akizungumza na BINGWA hivi karibuni, Kampira alisema kuwa kubwa lililowaangusha  msimu huu hasa katika mzunguko wa kwanza uliomalizika Novemba 7 ni kupungua kwa baadhi ya wachezaji wake aliokuwa nao katika ligi iliyopita, lakini pia changamoto nyingi pamoja na ushindani wa hali ya juu kutoka katika kila timu.

Alisema kuwa kutokuwepo kwa wachezaji hao kumevuruga kabisa mfumo wake hasa katika safu ya ushambuliaji na ulinzi, kwani kikosi chake kimeonekana kupwaya sana katika maeneo hayo.

Kampira alisema kuwa kwa sasa anaandaa ripoti ya kuwakabidhi viongozi wa timu hiyo, ili kuangalia wachezaji wanaoweza kuongezwa katika nafasi hizo ili kikosi kiwe na uhai kwenye mzunguko wa pili wa ligi.

“Ni kweli tumefanya vibaya tena tofauti na msimu uliopita, na hali hiyo imechangiwa na kuondoka kwa baadhi ya wachezaji wangu niliokuwa nao msimu iliopita, lakini tutafanya marekebisho na kuongeza wachezaji kwani tumepoteza mechi nyingi na hatutarajii hilo lijirudie tena mzunguko wa pili na kubaki katika ligi hiyo mzunguko wa pili,” alisema.

0 comments:

Post a Comment