VodaCom

Tangaza na gazeti la Bingwa.

NMB babu kubwa

Tangaza hapa huduma zako.

Commercial Bank of Africa

Tuna matumaini makubwa na huduma zako. Tangaza nasi.

AIRTEL huiweka dunia nzima karibu na watu

Haitoshi tu kusema AIRTEL YATOSHA. Inatosha kusema Airtel ni kila kitu.

TIGO, mtandao mkongwe zaidi nchini

TIGO ilionyesha njia. Sasa mawasiliano ni rahisi zaidi.

Sunday, November 10, 2013

Tambwe mguu ndani, nje Simba

NA ZAINAB IDDY


MSHAMBULIAJI wa Simba, Amisi Tambwe amesema hana muda mrefu kuitumikia Simba, kwani ameanza mazungumzo na timu moja ya Saudi Arabia.

Tambwe aliyasema hayo juzi kwenye mazungumzo maalumu saa chache kabla ya kuelekea Bujumbura, Burundi, baada ya kumalizika kwa mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu Bara.

Alisema kuna uwezekano mkubwa akavunja mkataba na Simba na huenda asionekane katika kikosi hicho katika  mzunguko wa pili, endapo mazungumzo kati ya meneja wake, Alphonce George Twagilamungu yatakwenda  vizuri na timu hiyo ya Saudi Arabia.

“Kuna taarifa nimezipata kutoka kwa meneja wangu, kuna timu imevutiwa na kiwango changu kutoka Saudi Arabia, ila bado tupo kwenye mazungumzo,” alisema.

Tambwe alisema anataka kutumia muda huu wa mapunziko akiwa Burundi, kukutana na meneja wake ili kujua hatima ya uwepo wake Simba.

“Kazi yangu ni mpira, hivyo nipo tayari kucheza katika timu yoyote itakayonihitaji ili mradi timu husika ifuate taratibu za mahali nilipo na itimize yale ninayoyahitaji,” alisema.

Mrundi huyo alisajiliwa na Simba msimu huu kwa mkataba wa miaka miwili akitokea klabu ya Vital’O ya Burundi, ambapo ameonesha uwezo mkubwa katika mzunguko wa kwanza uliomalizika hivi karibuni.

Tambwe ni kinara wa upachikaji wa mabao Ligi Kuu Bara msimu huu, ambapo hadi mzunguko wa kwanza unamalizika, straika huyo ametikisa nyavu mara 10.

Vita kali ya usajili Simba, Yanga

NA ABDUCADO EMMANUEL

KITENDO cha Yanga SC kumsajili kipa wa zamani wa Simba SC, Juma Kaseja, kimeonesha kuamsha vita kali ya usajili miongoni mwa timu hizo, lengo likiwa ni kubomoana.

Kwa mujibu wa kalenda ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), inaonesha kuwa dirisha dogo la usajili litafunguliwa rasmi Ijumaa ijayo na kufungwa Desemba 15 mwaka huu.

Ijumaa iliyopita saa 2 usiku, Yanga ilifanikiwa kuinasa saini ya Kaseja, kwa dau la Sh milioni 40, kwa mkataba wa miaka miwili, ambapo waliwapiku wapinzani wao wa jadi Simba, ambayo nayo ilikuwa vitani kumwania.

Simba ilipanga kumrudisha kundini, Kaseja licha ya kumnyima mkataba mpya msimu huu, kutokana na kipa  Mganda, Abel Dhaira kuboronga kwa kufungwa mabao ya kizembe kwenye mechi mbalimbali alizoichezea timu hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa za ndani kutoka Simba, zinasema kuwa mara baada ya Kaseja kusajiliwa Yanga, klabu hiyo imekuwa na vikao vizito juzi na jana ambapo wametoka na azimio la kuibomoa klabu ya Yanga.

“Baada ya kumkosa Kaseja, hivi sasa tutapambana kumsajili kipa aliyekalia kuti kavu ndani ya Yanga, Ally Mustafa ‘Barthez’, ili kuimarisha nafasi ya kipa ambayo imepwaya,” kilisema chanzo hicho.

Simba inaweza kufanikiwa kwenye jaribio lake hilo, kutokana na Barthez kuwa mbioni kutimka Yanga, kufuatia kuandamwa na mashabiki mara kwa mara, baada ya matokeo ya sare ya mabao 3-3 dhidi ya Simba, wakidai alihujumu mechi hiyo na kuachia mabao kizembe.

Pia suala la kuwekwa benchi nalo linachangia kwenye mbio hizo za Barthez kutaka kuikacha Yanga, huku akiona giza zaidi mara baada ya kutua kwa Kaseja, kwani aliwahi pia kumkimbia akiwa Simba kutokana na kuwekwa kwake benchi.

“Kama hiyo (kumchukua Barthez) haitoshi, tumepanga kuibomoa Yanga kwa kuchukua mshambuliaji wao mmoja ambaye ni noma kwa kupachika mabao hivi sasa, ila hatuko tayari kutangaza kwa sasa,” kilizidi kueleza chanzo hicho

Katika kuhakikisha wamedhamiria kuitikisa Yanga, tayari wameingia kwenye vita ya kumwania kiungo wa timu ya Ruvu Shooting, Hassan Dilunga, ambaye pia anawaniwa na Wanajangwani.

Simba imepanga kumsajili ili kuziba pengo la Haruna Moshi ‘Boban’ aliyehamia Coastal Union msimu huu.

Mbali na majina hayo pia lipo jina la kiungo mshambuliaji wa Yanga, Simon Msuva, ambaye naye anateswa na mashabiki wa Yanga, ambao humzomea kila akiwa dimbani, hii ni kutokana na kutomwamini kinda huyo aliyetokea Ruvu Shooting, huku pia suala la kuwa na mapenzi na Simba likionesha kumtesa zaidi.

Hali kama hiyo inamkumba kiungo mshambuliaji wa Simba, Harun Chanongo, ambaye aliondoshwa kikosini mara baada ya kuboronga kwenye mechi dhidi ya Yanga, akihusishwa na mapenzi ya dhati aliyokuwa nayo kwa Yanga.

Ambapo inasemekana ni mmoja wa wachezaji aliyehusika kuihujumu Simba kwenye mechi hiyo, kufuatia kocha wa timu hiyo, Abdallah ‘King’ Kibadeni kukiri baadhi ya nyota wake kuhusika. Inaelezwa kuwa nyota huyo amepanga kutimkia Yanga ili kuondokana na hali hiyo inayoendelea kumtesa, baada ya kuwekwa kando kwenye kikosi cha Simba.

Hii si mara ya kwanza kwa Simba na Yanga, kuvurugiana mipango ya usajili pamoja na kubomoana vikosi vyao, kwani msimu uliopita Yanga iliibomoa Simba, kwa kumsajili beki wake kisiki Kelvin Yondani, huku Simba ikimsajili beki wa Yanga, Amir Maftah misimu miwili iliyopita.

Familia yampeleka Kaseja Yanga

NA EZEKIEL TENDWA

LICHA ya Juma Kaseja kuwa radhi kujiunga na timu yake ya zamani, Simba baada ya mzunguko wa kwanza kumalizika, kikwazo kikubwa kilikuwa kwa familia yake iliyomtaka kujiunga na Yanga.

Familia ya Kaseja ilifikia uamuzi huo baada ya Simba kumtema kipa huyo na nahodha ya timu ya Taifa, ‘Taifa Stars’ kabla ya msimu huu kuanza licha ya kuichezea kwa mafanikio makubwa tangu ajiunge nayo.

Tayari Kaseja amesaini mkataba wa miaka miwili Yanga baada ya benchi la ufundi kumpendekeza asajiliwe wakiamini ataiokoa timu hiyo katika michuano ya kimataifa inayowakabili, kutokana na kipa huyo kuwa na uzoefu mkubwa.

Kabla ya kusajiliwa na Yanga, viongozi wa Simba walitaka kumrudisha katika dirisha dogo lakini familia yake ilimsihi asirudi tena kwenye timu hiyo na badala yake aende kwa watani wao wa jadi Yanga hatua ambayo Kaseja aliitekeleza.

Simba ilimuacha Kaseja kwa madai ya kushuka kiwango, wakiwa na jeuri ya kumtumia, Abel Dhaira na Andrew Ntala ambao hata hivyo wameonekana kutokuwa makini kama Kaseja.

Hii ni mara ya pili Kaseja kusajiliwa na mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Bara, ambapo kabla ya hapo alishaichezea timu hiyo msimu 2008/09 na baadaye kurejea tena Simba.

Baada ya kusajiliwa na Yanga, Kaseja anaungana na magolikipa wawili wa timu hiyo, Ali Mustafa ‘Barthez’ pamoja na Deogratias Munish ‘Dida’ ambao wote wamewahi kuichezea Simba kabla ya kujiunga na Yanga.

Azam, Coastal Union watunishiana misuli

NA ZAITUNI KIBWANA

TIMU za Azam na Coastal Union zinazoshiriki michuano ya Kombe la Uhai inayoshirikisha wachezaji wenye umri chini ya miaka 20 wa klabu za Ligi Kuu, wametunishiana misuli kwenye michezo ya ufunguzi wa mashindano hayo.

Ofisa habari wa Azam, Jafari Iddi aliliambia BINGWA kuwa kikosi chao kimeahidi ubingwa wa michuano hiyo, hivyo Coastal Union wajiandae kwa kichapo.

Wakati Jafari akiyasema hayo msemaji wa Coastal Union, Hafidhi Kido alisema kuwa mwaka huu wana vijana watakaoleta changamoto kwenye michuano hiyo.

Michuano hiyo mwaka huu itafanyika kwenye viwanja vya Karume na Azam Complex, Dar es Salaam.

Kundi A linaundwa na timu za Azam, Coastal Union, JKT Ruvu Stars, Mbeya City na Yanga, wakati kundi B ni Ashanti United, Mgambo Shooting, Oljoro JKT na Ruvu Shooting, Kagera Sugar, Mtibwa Sugar, Rhino Rangers na Tanzania Prisons ndizo zinazounda kundi C.

Kwa mujibu wa Ofisa Mashindano, Idd Mshangama, alisema kuwa mechi hizo za ufunguzi timu za Yanga na Mbeya City (saa 8 mchana- Karume).

Kundi B ni Ruvu Shooting na Ashanti United saa 4 asubuhi- Karume, Oljoro JKT na Simba saa 10 jioni- Karume

Benchi la ufundi Simba kuwasilisha ripoti wiki hii

NA EZEKIEL TENDWA

RIPOTI ya benchi ya ufundi la timu ya Simba, inatarajiwa kuwasilishwa kwa  kamati ya utendaji wiki hii.

Akizungumza jana, Ofisa habari wa Simba, Ezekiel Kamwaga alisema kuwa makocha wa timu hiyo wameahidi kuwasilisha ripoti kwa kamati ya utendaji wiki ili iweze kufanyiwa kazi.

Alisema kwamba baada ya kumalizika kwa mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu Tanzania bara na timu yao kumaliza wakiwa nafasi ya nne, walitoa muda kwa benchi lao la ufundi kuandaa ripoti hiyo ambayo wataiwasilisha ndani ya wiki hii.

“Baada ya kumalizika kwa mzunguko wa kwanza, tulitoa muda kwa benchi letu la ufundi kuandaa ripoti yao na mapendekezo yao ambapo ndani ya wiki hii wataiwasilisha nasi tutaifanyia kazi,” alisema.

Alisema baada ya kupata ripoti hiyo, wataifanyia kazi kwani lengo lao ni kuhakikisha mzunguko wa pili timu hiyo inafanya vizuri na kujikita kileleni mwa msimamo ambao kwa sasa unakaliwa na watani zao wa jadi Yanga.

Kocha Mgambo JKT alia na wachezaji

NA SALMA JUMA

KOCHA mkuu wa timu ya Mgambo JKT, Mohamed Kampira ameweka wazi sababu iliyopelekea timu yake kufanya vibaya katika mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu Bara msimu huu, kuwa ni kuondoka kwa baadhi ya wachezaji wake aliokuwa nao katika ligi iliyopita.

Mgambo wanashikilia mkia kwenye msimamo wa ligi hiyo wakiwa na jumla ya pointi 6, baada ya kushinda mchezo mmoja, kutoka sare mechi tatu na kupoteza mechi 9.

Akizungumza na BINGWA hivi karibuni, Kampira alisema kuwa kubwa lililowaangusha  msimu huu hasa katika mzunguko wa kwanza uliomalizika Novemba 7 ni kupungua kwa baadhi ya wachezaji wake aliokuwa nao katika ligi iliyopita, lakini pia changamoto nyingi pamoja na ushindani wa hali ya juu kutoka katika kila timu.

Alisema kuwa kutokuwepo kwa wachezaji hao kumevuruga kabisa mfumo wake hasa katika safu ya ushambuliaji na ulinzi, kwani kikosi chake kimeonekana kupwaya sana katika maeneo hayo.

Kampira alisema kuwa kwa sasa anaandaa ripoti ya kuwakabidhi viongozi wa timu hiyo, ili kuangalia wachezaji wanaoweza kuongezwa katika nafasi hizo ili kikosi kiwe na uhai kwenye mzunguko wa pili wa ligi.

“Ni kweli tumefanya vibaya tena tofauti na msimu uliopita, na hali hiyo imechangiwa na kuondoka kwa baadhi ya wachezaji wangu niliokuwa nao msimu iliopita, lakini tutafanya marekebisho na kuongeza wachezaji kwani tumepoteza mechi nyingi na hatutarajii hilo lijirudie tena mzunguko wa pili na kubaki katika ligi hiyo mzunguko wa pili,” alisema.

Kung Fu Mbagala kufanya mashindano mara kwa mara

NA ZAINAB IDDY

UONGOZI wa klabu ya Kung Fu ya Mbangala jijini Dar es Salaam, umepanga programu ya kufanya mashindano ya mara kwa mara, kwa lengo la kuendeleza mchezo huo nchini.

Abdallah Nyoni ni Katibu Mkuu wa klabu hiyo, aliliambia BINGWA kwamba mashindano hayo yatasaidia kupata vipaji ambavyo vitawasaidia katika mashindano mbalimbali.

“Hiyo ni moja ya maandalizi ya kuwaandaa wachezaji kwa ajili ya mashindano mbalimbali mwakani, hivyo tunajipanga mapema,” alisema.

Alisema mwakani kutakuwa na mashindano mbalimbali ndani na nje ya nchi, ndiyo maana wameamua kutengeneza timu yao kupitia mashindano hayo.

Nyoni alisema mbali na programu hiyo, kutakuwa na mazoezi ya kila wiki ambayo yatawawezesha wachezaji kujiweka sawa na kuwa tayari muda wowote kushiriki michuano itakayoandaliwa na klabu nyingine.

“Tutahakikisha tunakuwa mfano wa kufanya vema katika mchezo huo nchini, ndiyo maana tunafanya mambo yote hayo,” alisema.