Sunday, August 4, 2013

Utata mafuta ya ubuyu

Vita ya uwanjani imetimia

NA GABRIEL MUSHI
SIKU moja baada ya Taasisi ya Saratani ya Ocean Road, kutoa tamko linaloeleza kuwa mafuta ya ubuyu hayana madhara katika mwili wa binadamu yakitumiwa vizuri, Serikali imekanusha hilo kwa kuwaonya wananchi wasiyatumie kwa sababu ni hatari.

Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Seif Rashid, jana alitangaza kuwa mafuta hayo si salama na kusisitiza kuwa huo ndiyo msimamo wa Serikali kuhusu mafuta hayo, hivyo wananchi waamue wenyewe kuyatumia au kutoyatumia.

Dk. Rashid alitoa kauli hiyo wakati akijibu maswali ya waandishi wa habari baada ya kufungua semina ya siku mbili, iliyoandaliwa na Mamlaka ya Chakula na Dawa nchini (TFDA) na Shirika la Afya Duniani (WHO).

Alisema kwa kuwa tayari TFDA imeshatoa tamko kuwa mafuta hayo si salama, hivyo wananchi ni hiari yao kutekeleza agizo hilo au kutolitekeleza.

“Tayari chombo cha serikali ambacho kina mamlaka juu ya hili kimeshatoa tamko, hivyo ni hiari ya wananchi kuamua wenyewe kuyatumia au kutoyatumia.

“Kwa sababu ni sawa na sigara, tumesema kabisa sigara inasababisha saratani na matatizo mengine tukaweka na onyo kwenye kasha la sigara zenyewe, hivyo ni hiari kutumia au kutotumia.

Alisema madhara yaliyo kwenye mafuta ya ubuyu yamegundulika hivi karibuni, baada ya kufanyiwa uchunguzi ambao ulichukua muda mrefu na hivyo kuchelewa kutangaza madhara yake.

Akizungumza kabla ya kumkaribisha Dk. Rashid, Mkurugenzi Mtendaji wa TFDA, Hiiti Sillo, alisema semina hiyo inashirikisha nchi 16 zilizopo kusini mwa Jangwa la Sahara.

Alisema imeandaliwa kwa ajili ya kuwapatia wakaguzi mbinu mpya za kudhibiti dawa bandia ambazo zinasababisha madhara kwa binadamu.

“Tatizo la dawa bandia linatakiwa kushirikiana na nchi nyingine, ndiyo maana mafunzo haya yatatumika kujenga uhusiano pamoja na kubadilisha uzoefu namna ya kukamata dawa hizo,” alisema.

Mwakilishi wa Shirika la Afya kutoka Geneva, Dk. Michael Deats, alisema tatizo la dawa bandia ni tatizo sugu linalozisumbua nchi za Bara la Afrika.

Hivi karibuni, TFDA ilipiga marufuku matumizi ya mafuta ya ubuyu kwa madai kuwa yanasababisha saratani, tamko ambalo lilipingwa vikali na wataalamu wa tiba mbadala.

Pamoja na hilo, juzi Taasisi ya Saratani ya Ocean Road  ilitangaza kuwa mafuta hayo ni salama iwapo yakitumiwa vizuri, tamko hilo pamoja na mwendelezo wa malalamiko kutoka kwa wananchi na wataalamu mbalimbali, limekuwa likizua utata kwa kuwa kila upande unaonekana kutoa msimamo wake jambo ambalo limeibua mjadala katika jamii.

0 comments:

Post a Comment